2 Peter 2

Walimu Wa Uongo Na Uangamivu Wao

1Lakini pia waliinuka manabii wa uongo miongoni mwa watu, kama vile watakavyokuwako walimu wa uongo miongoni mwenu. Wataingiza mafundisho yasiyopatana na kweli kwa siri, hata kumkana Bwana wa pekee aliyewanunua, na hivyo kujiletea wenyewe maangamizi ya haraka. 2Hata hivyo, wengi watafuata njia zao za ufisadi, na kwa ajili yao njia ya kweli itatukanwa. 3 aNao katika tamaa zao mbaya, walimu hawa watajipatia faida kwenu kwa hadithi walizotunga wenyewe. Lakini hukumu imekwisha kutangazwa dhidi yao tangu zamani, wala uangamivu wao haujalala usingizi.

4 bKwa maana, kama Mungu hakuwasamehe malaika walipotenda dhambi, bali aliwatupa kuzimu
Kuzimu hapa linalotokana na neno Tartarus la Kiyunani; maana yake ni kule ndani sana katika mahali pa mateso kwa watu waliopotea.
katika vifungo vya giza wakae humo mpaka ije hukumu;
5 dkama hakuusamehe ulimwengu wa kale alipoleta gharika juu ya watu wale wasiomcha Mungu, bali akamhifadhi Nuhu, mhubiri wa haki, pamoja na watu wengine saba; 6 ekama aliihukumu miji ya Sodoma na Gomora kwa kuiteketeza kwa moto ikawa majivu, na kuifanya kuwa kielelezo kwa yale yatakayowapata wale wasiomcha Mungu; 7 fna kama alimwokoa Lutu, mtu mwenye haki, ambaye alihuzunishwa na maisha machafu ya watu wapotovu 8 g(kwa sababu yale matendo mapotovu aliyoyaona na kuyasikia huyo mtu mwenye haki alipoishi miongoni mwao yalimhuzunisha siku baada ya siku): 9 hikiwa hivyo ndivyo, basi Bwana anajua jinsi ya kuwaokoa wamchao Mungu kutoka majaribu, na kuwaweka waasi katika adhabu hadi siku ya hukumu. 10 iHii ni hakika hasa kwa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kudharau mamlaka.

Kwa ushupavu na kwa kiburi, watu hawa hawaogopi kunena mabaya dhidi ya viumbe vya mbinguni.
11Lakini hata malaika, ingawa wana nguvu na uwezo zaidi, hawaleti mashtaka mabaya dhidi ya viumbe kama hao mbele za Bwana. 12 jLakini watu hawa hukufuru katika mambo wasiyoyafahamu. Wao ni kama wanyama wasio na akili, viumbe wanaotawaliwa na hisia za mwili, waliozaliwa ili wakamatwe na kuchinjwa. Hawa nao kama wanyama wataangamizwa pia.

13 kWatalipwa madhara kwa ajili ya madhara waliyowatendea wengine. Huhesabu kuwa ni fahari kufanya karamu za ulevi na ulafi mchana peupe. Wao ni mawaa na dosari, wakijifurahisha katika anasa zao wanaposhiriki katika karamu zenu. 14 lWakiwa na macho yaliyojaa uzinzi, kamwe hawaachi kutenda dhambi. Huwashawishi wale wasio imara. Wao ni hodari kwa kutamani; ni wana wa laana! 15 mWameiacha njia iliyonyooka, wakapotoka na kuifuata njia ya Balaamu mwana wa Beori aliyependa mshahara wa uovu. 16 nLakini kwa ajili ya uovu wake, alikemewa na punda, mnyama asiyejua kusema, akaongea akitumia sauti ya mwanadamu na kuzuia wazimu wa huyo nabii.

17 oWatu hawa ni chemchemi zisizo na maji, na ukungu upeperushwao na tufani. Giza nene limewekwa tayari kwa ajili yao. 18 pKwa maana wao hunena maneno makuu mno ya kiburi cha bure, na kwa kuvutia tamaa mbaya za asili ya mwili, huwashawishi watu ambao ndipo tu wamejiondoa miongoni mwa wale wanaoishi katika ufisadi. 19 qHuwaahidi uhuru hao waliowanasa, wakati wao wenyewe ni watumwa wa ufisadi: kwa maana mtu ni mtumwa wa kitu chochote kinachomtawala. 20 rKama wameukimbia upotovu wa dunia kwa kumjua Bwana wetu na Mwokozi Isa Al-Masihi, kisha wakanaswa tena humo na kushindwa, hali yao ya mwisho ni mbaya zaidi kuliko ile ya kwanza. 21 sIngelikuwa afadhali kwao kama wasingeliijua kamwe njia ya haki, kuliko kuijua kisha wakaiacha ile amri takatifu waliyokabidhiwa. 22 tImetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli isemayo: “Mbwa huyarudia matapiko yake mwenyewe,” tena, “Nguruwe aliyeoshwa hurudi kugaagaa matopeni.”
Copyright information for SwhKC